Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamehitimisha Mkutano wa 41 wa Kawaida wa Jumuiya hiyo uliofayika kwa siku mbili Lilongwe nchini Malawi. 

Katika siku ya pili na ya mwisho ya Mkutano huo, Wakuu hao wamesani nyaraka za kisheria 4  ambazo ni Itifaki ya Takwimu, Mkataba wa Marekebisho ya Itifaki ya Nishati ya SADC na Marekebishio ya Kiambatisho Na.1 cha Itifaki ya Nishati ya SADC, Mkataba wa kuboresha Itifaki ya SADC ya Silaha na Mkataba kuhusu hadhi ya Jeshi la dharura la SADC.

Akisoma tamko la pamoja, Katibu Mtendaji anayemaliza muda wake Dkt. Stergomena Tax amesema Wakuu hao wa Nchi na Serikali wamemthibitisha na kumuapisha Katibu Mtendaji mpya wa Sekretarieti ya Jumuiya hiyo Bw. Elias Mpedi Magosi kutoka Jamhuri ya Botswana ambaye anakuwa Katibu Mtendaji wa 7 baada ya aliyekuwa Katibu Mtendaji  Dkt. Stergomena Tax kumaliza muda wake wa miaka 8 ya  utendaji katika SADC.

Dkt. Tax ameongeza kuwa Wakuu hao wa Nchi na Serikali wameendelea kusisitiza kuondolewa kwa vikwazo vya Kiuchumi dhidi ya Zimbabwe bila masharti na kuiunga mkono Zimbabwe kwa jitihada zake za kuendelea kuimarisha uchumi wake.    

Vilevile, Wakuu hao wa Nchi na Serikali wamewapongeza Wananchi na Serikali ya Jamhuri ya Zambia kwa kufanya uchaguzi Mkuu na kumpongeza Rais Mteule Mhe. Hakainde Hichilema kwa kuibuka mshindi.

Viongozi hao wa SADC wamepokea taarifa kuhusu hali ya Usalama katika jimbo la Cabo Delgado Kaskazini mwa Msumbiji na kupongeza Nchi wanachama wa SADC kwa michango yao ya kifedha iliyowezesha kupelekwa kwa Jeshi la Dharura la SADC nchini Msumbiji.

Mkutano huo wa 41 pia umeridhia mabadiliko ya Jukwaa la Bunge la SADC kuwa Bunge la SADC la ushauri na majadiliano.

Dkt. Tax amesema Wakuu hao wa Nchi na Serikali wa SADC kwa kauli moja wamekubaliana kuwa Mkutano wa 42 wa Kawaida  wa Jumuiya hiyo utafanyika nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Agosti 2022.

Nje ya Mkutano huo, Mhe. Rais Samia amekutana na kufanya mazungumzo na Rais mstaafu wa Malawi Mhe.  Joyce Banda.

Mhe. Rais Mstaafu Joyce Banda amempa pole Mhe. Rais Samia kufuatia msiba wa Hayati Rais Magufuli na kumpongeza kwa kushika nafasi ya Urais, ambapo amemuahidi kumpa ushirikiano akiwa Rais mstaafu mwanamke.

Kwa upande wake Mhe. Rais Samia amemshukuru Rais Mstaafu Banda na kuahidi kuendeleza ushirikiano wa kidugu na wa kihistoria kati ya Tanzania na Malawi.

Mhe. Rais Samia amerejea nchini na kupokewa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango pamoja na viongozi mbalimbali  katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar