Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiongoza Viongozi mbalimbali na
Wananchi kuaga Mwili wa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa marehemu Elias John Kwandikwa katika Viwanja vya Karimjee
Jijini Dar es Salaam leo tarehe 06, Agosti 2021.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiifariji Familia ya aliyekuwa
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa marehemu Elias John
Kwandikwa baada ya kuongoza Viongozi mbalimbali na Wananchi kuaga Mwili wa Hayati
Kwandikwa katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam leo tarehe
06, Agosti 2021.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema kifo cha marehemu Kwandikwa kimeacha simanzi na pengo kubwa si kwa familia pekee bali pia kwa Serikali na Taifa kwa ujumla.
Raisi Samia ameyasema hayo leo tarehe 06 Agosti, 2021 wakati akiwaongoza viongozi mbalimbali na waombolezaji kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Marehemu Elias John Kwandikwa.
Amesema Serikali imempoteza mtumishi na kiongozi mwadilifu, makini,
shupavu na mchapakazi hodari.
Aidha, Mhe. Rais Samia amewashukuru viongozi wa dini kwa kuongoza ibada
ya kumuaga marehemu Kwandikwa ambapo mahubiri yao yametoa faraja na kukumbusha
kuwa wanadamu duniani wanapita, hivyo kutakiwa kuishi kwa wema na kutenda yale
ya kumpendeza Mungu.
Shughuli za kuaga mwili wa Marehemu Kwandikwa zimefanyika katika viwanja
vya Karimjee Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa
Serikali akiwemo Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango, Rais wa Zanzibar Mhe.
Dkt. Hussein Mwinyi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdallah, Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson,
Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi
Hussein Kattanga, Katibu Mkuu Kiongozi-Zanzibar Mhandisi Zena Said pamoja na
viongozi wengine wa vyama vya Siasa na
Serikali.
“Bwana ametoa, Bwana
ametwaa, Jina lake lihimidiwe”




0 Maoni