Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na kumpongeza Rais
Mpya wa Zambia Mhe. Hakainde Hichilema, mara baada ya kuapishwa kuwa Rais wa 7
wa Zambia katika Uwanja wa Taifa wa Mashujaa (National Heroes Stadium) Jijini
Lusaka Zambia leo Agosti 24,2021.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 24 Agosti, 2021
amehudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Saba wa Zambia Mhe. Hakainde
Hichilema zilizofanyika katika Uwanja wa Taifa wa Mashujaa (National Heroes Stadium), Jijini Lusaka.
Mhe.
Rais Samia amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Hichilema ambapo amempongeza kwa ushindi
wa nafasi ya Urais pamoja na kuwapongeza wananchi wa Zambia kwa kufanya
uchaguzi wa amani. Mbali na salamu za pongezi amemuahidi Rais Hichilema
kuendeleza ushirikiano na uhusiano wa kihistoria uliopo baina ya Tanzania na
Zambia.
Katika mazungumzo hayo Mhe.
Rais Samia na Mhe. Rais Hichilema wamezungumzia umuhimu wa kuihuisha mikutano
ya Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) ili kuweza kubaini fursa
mbalimbali za ushirikiano ikiwemo kuimarisha ushirikiano uliopo wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia
(TAZARA) na Bomba la mafuta la Tanzania na Zambia (TAZAMA).
Lengo la mikutano hii mbali
na kuibua fursa mbalimbali pia ni kuweza kutatua changamoto ziliopo katika
sekta mbalimbali ili ziweze kuwa na tija na kutoa manufaa kwa
nchi mbili hizo.
Mhe. Rais Samia ameeleza
umuhimu wa kukuza biashara baina ya Tanzania na Zambia ili uende sambamba na
uhusiano wa kihistoria tuliokuwa nao.
Mhe. Rais Samia ameiomba Serikali ya
Zambia kuendelea kutumia Bandari ya Dar es Salaam kupitishia mizigo
yake, ombi ambalo lilikubaliwa na kuungwa mkono na Mhe. Hichilema.
Kwa upande wake Mhe. Rais Hichilema ametoa salamu
za rambirambi kwa Mhe. Rais Samia na Watanzania wote kwa kumpoteza Hayati Mhe.
Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Aidha, Mhe. Rais Hichilema amemshukuru Mhe.
Rais Samia kwa kushiriki katika sherehe za uapisho na kuahidi kufanya kazi na
nchi zote jirani na utayari wake wa kushirikiana na nchi hizo katika kudumisha
urafiki wa kidugu na kihistoria kwa maendeleo ya wananchi wake.
Mhe. Rais Hichilema mesisitiza umuhimu wa
kukuza biashara kama njia ya kujenga
uchumi wa nchi yake na kuinua maisha ya wananchi wake. Vilevile alizungumzia
umuhimu wa Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano hususani kwenye suala zima
la kushughulikia changamoto zinazokwamisha ushirikiano ambapo
ameahidi kutoa msukumo wa kisiasa kuhakikisha mikutano hiyo inafanyika mara kwa
mara.
Vilevile, Mhe. Rais
Hichilema amemshukuru Mhe. Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Kikwete kwa
kazi nzuri aliyoifanya na uongozi uliotukuka katika kusimamia timu ya Waangalizi wa
Uchaguzi kutoka Jumuiya ya Madola na ameeleza kuwa
yeye kama kiongozi mgeni yupo tayari kujifunza kwa viongozi wakongwe.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Samia
amemualika Mhe. Rais Hichilema kufanya ziara
Nchini Tanzania, na Mhe. Rais Hichilema amekubali mwaliko huo.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiszungumza na Rais
Mpya wa Zambia Mhe. Hakainde Hichilema, mara baada ya kuapishwa kuwa Rais wa 7
wa Zambia katika Uwanja wa Taifa wa Mashujaa (National Heroes Stadium) Jijini
Lusaka Zambia leo Agosti 24,2021
0 Maoni