Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Oman nchini Balozi  Ali Bin Abdallah Bin Salim Al Mahrouqi aliyemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini.

Katika mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Dodoma, Balozi Al Mahrouqi amempongeza Rais Samia kwa utawala wake na kuishukuru Serikali ya Tanzania  kwa ushirikiano mkubwa alioupata wakati alipokuwa akitekeleza majukumu yake.

Amesema Tanzania na Oman zina uhusiano mzuri na wa muda mrefu hivyo kuomba kuendelezwa kwa ajili ya maslahi ya nchi zote mbili pamoja na kuimarishwa biashara.

Nae Rais Samia amemhakikishia Balozi Al Mahrouqi kuwa Tanzania itaendeleza na kudumisha ushirikiano wake na Oman kwa maslahi ya nchi zote mbili.

Amemjulisha Balozi huyo kuwa kwa sasa Tanzania inapitia sheria na sera zake mbalimbali za biashara ili kujenga mazingira mazuri zaidi ya biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na  kuongeza ufanisi katika viwanja vya Ndege na Bandari ili kurahisisha ufanyaji biashara baina ya nchi hizi mbili.

Pia, Rais amezitaka Tume za pamoja kati ya Tanzania na Oman kukutana na kuzungumza ili kuimarisha mambo mbalimbali baina ya nchi hizo.

 Rais Samia amemshukuru na kumpongeza Balozi Al Mahrouqi kwa kazi nzuri ya uwakilishi wake hapa nchini katika kipindi cha miaka 4 kwa kudumisha uhusiano kati ya Oman na Tanzania.