NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ameitaka wizara ya Biashara na Maendeleo ya
Viwanda Pemba kuendelea kuzitangaza fursa zinazopatikana katika eneo la
Chamanangwe Kisiwani humo lililotengwa na Serikali kwa ajili ya uwekezaji
ili kuwawezesha wawekezaji wazalendo na wa kigeni kuja kuwekeza.
Akiwa katika ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa viwanda katika eneo hilo , Balozi Mbarouk amesema kutangazwa eneo hilo kutasaidia kuvutia wawekezaji na hivyo kutoa ajira kwa vijana na kupunguza hali ya umaskini wa kipato.
Naye Afisa Mdhamini Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Ali Suleiman amemwambia Naibu Waziri kwamba mbali na ujenzi wa kiwanda cha Maji katika eneo hilo , pia wawekezaji wengine wanatarajia kujenga kiwanda cha mwani na chumvi.
Akitoa maelezo ya ujenzi wa kiwanda cha Maji Fundi Victor Bilali Rashid amesema kazi zinaendelea vizuri huku akitaja changamoto inayowakabili na uhaba wa saruji.
Awali balozi Mbarouk amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib ambaye amemtaka Naibu Waziri huyo kutumia nafasi yake kuzitangaza fursa za uwekezaji zilizopo Kisiwani Pemba.
.mwisho.





0 Maoni