Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amewahimiza wananchi kujitokeza kwa hiari na kupata Chanjo ya UVIKO19 hasa Wazee kwa kuwa salama na imethibitishwa na Watalaam wa Afya.

Mwanaidi ametoa kauli hiyo Wilayani Songea Mkoani Ruvuma wakati wa ziara yake mkoani humo kukagua huduma za matibabu kwa Wazee katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.

Amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii na Maafisa Maendeleo ya Jamii kuendelea kutoa elimu na kuwahamasisha Wazee kuanzia umri wa miaka 50 kujitokeza kwa hiari yao kupata Chanjo ya UVIKO19.

"Awamu hii ya utoaji wa Chanjo ya UVIKO19 tumewapa kipaumbele Wazee kuanzia miaka 50 kupata Chanjo ya UVIKO19 ili kusaidia kupata kinga itakayowalinda na maambukizi ya Virusi vya Corona" alisema Mhe. Mwanaidi
Aidha, Mhe. Mwanaidi amewahimiza wanandoa walio na umri wa miaka 50 na kuendelea kuhimizana kupata Chanjo ya UVIKO19 ili waweza kujikinga na Virusi vya Corona.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Ruvuma Mariam Juma amesema kuwa wataendelea kuhamasisha jamii hasa kundi la wazee na watu wenye magonjwa sugu kujitokeza kwa hiari yao kupata Chanjo ya UVIKO19.