Na mwandishi wetu

Mkuu wa wilaya ya Mjini Rashid Simai  Msaraka  ametoa wiki moja kwa wafanyabiashara wa vifaa mbali mbali wa maeneo ya Mlandege Mjini Unguja, kuondoa sehemu ya mapaa ya maduka yao  yaliyozidi pembezoni mwa barabara na kusababisha kero kwa Wananchi

.Akizungumza na wafanyabiashara  hao, Mkuu wa  wilaya amesema kwa sasa  maduka hayo yamekuwa yakileta usumbufu  kwa wanaokwenda kwa miguu na hata wale  ambao wanaopaki  gari  zao hali inayoweza  kusababisha ajali kwa wananchi .

Amesema endapo wafanyabiashara hao wataondoa sehemu ya mapaa yaliyozidi kunaweza kupatikana  nafasi kubwa ya waendao kwa miguu na hata sehemu ya kupaki Magari na kuondoa msongamano wa magari katika maeneo hayo.

Nao baadhi ya wafanyabiashara wa maeneo hayo, wameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwapa muda wa wiki moja kwaajili ya kufanya matayarisho ya kuondoa vifaa vyao katika maduka hayo kwa kuwa kwa sasa hawajiandaa kutafuta maeneo mengine.

Aidha wafanyabiashara hao wamesema kuwa  wapo tayari   kufuata maagizo yaliyotolewa na serikali na kuhakikisha kuwa watabomoa  vipaa hivyo ili kuondosha usumbufu unaojitokeza mara kwa mara kwa watu wanaotumia maeneo hayo.