Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk ameitaka jamii kuzitumia vyema rasilimali za bahari pamoja na kuzilinda ikizingatiwa ni vyanzo muhimu katika kuelekea uchumi wa buluu na ukuaji wa uchumi wa nchi.

Ushauri huo umetolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, Moh’d Mkobani wakati wa uzinduzi wa kampeni ya uhifadhi wa Matumbawe inayotekelezwa na Jumuiya ya Kwanini Foundation, amesema matumizi sahihi ya rasilimali za bahari huchochea ukuwaji wa uchumi wa nchi na wananchi.

Nao Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kwanini Foundation pamoja na Mkuu wa Doria za bahari kutoka Wizara ya Uchumi wa Buluu wamesema kampeni hiyo itasaidia kuongezeka mazao ya baharini ikiwemo samaki.

Awali Afisa Mdhamini wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Thabit Othamna amezitaka asasi za kiraia kuendelea kushirikiana na Serikali kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.