Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wamesomewa upya mashtaka sita yakiwemo ya kufadhili vitendo vya ugaidi na kukusanya pesa za kufanya vitendo hivyo.

Mashtaka mengine ni kukutwa na silaha aina ya bastola na kukutwa na sare za jeshi kinyume cha sheria.

Kati ya mashtaka hayo sita, Mbowe anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kula njama na kufadhili fedha kwa ajili vitendo vya kigaidi.

Mshtakiwa Mbowe na wenzake watatu wamesomewa upya mashtaka yao hii leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambayo ni kula njama na tuhuma za Ugaidi ambayo waliyatenda kati ya Mei 1 na August 1, 2020 maeneo ya Moshi, Dar es Salaam, Morogoro na Arusha.

Mbali na Mbowe, ambaye ni mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo, washtakiwa wengine ni Halfan Hassa, Adam Kasekwa na Mohammed Lingwenya.

Washtakiwa baada ya kusomewa amshtaka hayo hawakutakiwa kujibu chochote ambapo Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 13, 2021 itakapotajwa.

Washtakiwa hao wanaotetewa na jopo la mawakili tisa wakiongozwa na Peter Kibatala wamerudishwa rumande, kwakuwa mashtaka yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.