Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman ameitaja Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia wazee na watoto katika orodha ya taasisi zisizozingatia nidhamu katika matumizi ya fedha za Serikali.

Amesema hayo leo katika ziara yake kwenye Hospital ya Rufaa ya Mnazi Moja ambapo amemuagiza Waziri wa wizara hiyo, Nassor Mazrui kuhakikisha dawa na Vifaa tiba vinavyonunuliwa viwe vinaendana na Thamani halisi ya Fedha inayotumika.

Mhe. Hemed amesema Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais Dkt. Mwinyi imedhamiria kudhibiti matumizi ya Fedha za Serikali na itakapobidi haitasita kubadilisha baadhi ya sheria ili kufanikisha lengo hilo.

Pamoja na hayo ameeleza kusikitishwa kwa kusuasua kwa huduma ya upatikanaji wa mashuka kwa wakati kulikosababishwa na kuharibika kwa kifaa cha mashine ya kufulia, kifaa ambacho harama yake haizidi sh. Laki Nne.

Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Hopital ya Rufaa ya Mnazi Mmoja Dkt. Msafiri Marijani amemueleza Mhe. Hemed kuwa wanakabiliwa na changamoto tofauti ikiwemo upungufu wa wataalamu wa kada mbali mbali, uhaba wa idadi ya Vyumba vya kuendesha matibabu ya upasuaji pamoja na upungufu wa Vitendanishi kwa ajili ya kufanya vipimo katika maabara.