KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi- CCM -Wilaya ya Wete
imeelezea kusikitishwa na kitendo cha kutelekezwa boti ya wagonjwa
(AMBULANCE BOAT) iliyotolewa na Serikali kwa ajili ya kutoa huduma za
mama na mtoto kutoka maeneo ya visiwa vidogo vidogo kwenda katika hospitali
kubwa na kuagiza aliyehusika na kitendo hicho akamatwe na afikishwe
kwenye vyombo vya sheria.
Ziara ya kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi -CCM-Wilaya hiyo imeagiza boti hiyo kufanyiwa matengenezo ili ianze kutoa huduma kwa wananchi, ambapo Katibu wa CCM Wilaya hiyo Salim Khamis Haji ametoa muda wa wiki mbili kwa taasisi husika kuwasilisha taarifa sahihi juu ya Boti hiyo , kwani chama hakiwezi kukaa kimiya wakati fedha za Serikali zinapotea .
Kapteni wa Boti hiyo Dawa Hamad Shoka amesema boti imeshindwa kutoa huduma kutokana na kukosa mafuta huku Afisa Kinga Wizara ya Afya Pemba Ramadhan Bilali amesema baada ya ugatusi bado boti hiyo haijarejeshwa wizarani.
Mkuu wa Wilaya ya Wete Bi Mgeni Khatib Yahya ameahidi kuwasilisha taarifa ndani ya Wiki mbili kama ilivyoagizwa na Chama.
Boti hiyo ilikabidhiwa serikalini mwaka 2019 hadi sasa imefanya safari za katika visiwa vidogo vidogo mara tatu jambo ambalo linawafanya wananchi wa visiwani kuendelea kupata shida hasa mama wajawazito




0 Maoni