Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Dkt. Doroth Gwajima ameliagiza Jeshi la Polisi pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini  (Takukuru)  kumkamata na kumhoji mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima ili athibitishe kauli anazozitoa dhidi ya Serikali na viongozi  kuhusu chanjo ya Covid-19.

Dkt. Gwajima amesema, Askofu Gwajima amekuwa akitoa taarifa za kupotosha kwa makusudi jambo linaloivuruga wizara yake na Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Kwa muda sasa  Askofu Gwajima kupitia ibada zake anazoziendesha kupitia kanisa lake la Ufufuo na Uzima licha ya kuhubiri mambo mengine ya kiimani lakini  amekuwa akisisitiza kuwa hatakubali kupatiwa chanjo ya kukabiliana na Uviko-19 na kuwataka waumini wake kutojitokeza kwenda kuchanja.