Msimamizi wa Chanjo ya Kipindupindu Unguja Dkt. Fadhil Mohammed Abdalla akielezea  azma ya serikali juu ya Chanjo ya kipindupindu pamoja na umuhimu wa Chanjo hiyo katika mafunzo kwa Waandishi wa habari yaliyofanyika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Unguja.

Na mwandishi wetu

Msimamizi wa Chanjo ya Kipindupindu Unguja Dkt. Fadhil Moh’d amesema chanjo ya kipindupindu haina mahusiano na chanjo ya Corona na haina madhara yoyote kwa binadamu.

Ameyasema hayo kwenye Ukumbi wa Sanaa Rahaleo wakati alipokuwa akitoa mafunzo kwa Waandishi wa Habari kuhusu Umuhimu wa kumaliza Dozi ya Pili ya chanjo hiyo.

Ameeleza kuwa azma ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar juu ya chanjo ya Kipindupindu inayotolewa kwa njia ya matone ni kutokomeza kabisa ugonjwa huo nchini hivyo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo.

Aidha Dk. Fadhili amewasihi wananchi kuachana na uvumi kuhusu usalama wa chanjo hiyo, amesema ni salama.

Akiwasilisha mada kuhusu Umuhimu wa Chanjo ya kipindupindu Dozi ya Pili  Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Afya, Halima Khamis amesema atakaemaliza dozi kamili ya chanjo hiyo ataepukana na ugonjwa huo kwa muda mrefu.

Amewataka wananchi kuendelea kufuata kanuni za kujikinga na maradhi ya kipindupindu ili kuhakikisha Zanzibar inatokomeza kabisa ugonjwa huo.

Hata hivyo amewasisitiza waandishi wa habari kuwahamasisha  wananchi kujitokeza kwa wingi katika awamu ya pili ya chanjo ya kipindupindu ambayo imeanza kutolewa jana hadi  11/08/2021.

Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Afya Halima Khamis akiwasilisha mada kwa Waandishi wa habari (hawamo pichani)  kuhusu umuhimu wa Chanjo ya Kipindupindu Dozi ya pili, iliyoanza kutolewa agosti 8 mwaka huu kwa shehia ambazo  hukumbwa na kipindu pindu mara kwa mara hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Unguja.

Afisa Afya, Muhsini Haji Makame akitolea ufafanuzi baadhi ya maswali ya waandishi wa habari mara baada ya kuwasilishwa mada ya Umuhimu wa Chanjo ya Kipindupindu dozi ya pili iliyoanza kutolewa agosti 8 mwaka huu kwa shehia ambazo  hukumbwa na kipindupindu mara kwa mara katika mafunzo ya waandishi wa Habari yaliyofanyika katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Unguja.