Na mwandishi wetu
Madereva wa Bodaboda
Visiwani Zanzibar wametakiwa kufuata Sheria Za Usalama barabarani ili kuepusha
ajali na vifo vilivyoshamiri chanzo ikiwa kutofuatwa kwa Sheria za Usalama
Barabarani.
Rai hiyo imetolewa leo
na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la
Taifa la Usalama Barabarani, Khamis Hamza Chilo wakati wa kikao na madereva
bodaboda wa Mkoa wa Mjini Magaharibi ambacho pia kilihudhuriwa na uongozi wa Jeshi
la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi.
“Serikali yenu Sikivu
chini ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi iko
katika mchakato ili mruhusiwe kutoa huduma za usafiri katika maeneo
mbalimbali ya Zanzibar sasa nawaomba muanze kujifunza na kufuata sheria za
usalama barabarani ili tunayoona yanayotokea kule Bara yasitokee huku.” alisema
Naibu Waziri Chilo
“….kuna mambo kadhaa
huku mmeshaanza kuhusishwa nayo kabla hata hamjaruhusiwa nawaombeni jiepusheni
na mambo hayo lengo la serikali ni kuwatengenezea mazingira mazuri ya kujiajiri
sasa ushiriki katika uhalifu yakiwemo matendo ya uporaji, kukata watu mapanga
sio jambo nzuri, jueni tu jeshi la polisi liko macho na halitosita kuwachukulia
hatua pindi mtakapobainika kujihusisha na matendo ya uhalifu” aliongeza Naibu
Waziri Chilo
Akizungumzia takwimu
za ajali za bodaboda, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna
Msaidizi wa Polisi Awadh Juma Haji amesema kumekuwepo na kupungua kwa ajali za
bodaboda na vifo kutokana na elimu inayotolewa kwa madereva hao wa bodaboda
lengo ni kuhakikisha utii wa sheria bila shuruti.
“Mwaka huu tuna ajali
17, watu waliofariki mwaka jana ni watu 18 na mwaka huu tuna vifo 17 huku
upungufu ukiwa ni mtu mmoja, lakini ajali zilizosababisha majeruhi kwa mwaka
jana ni ajali 19 na mwaka huu ni ajali 6 kwa hiyo kuna upungufu wa ajali 15,
watu waliojeruhiwa mwaka jana watu 37 na mwaka huu ni watu 6
kwahiyo tunaona kuna kushuka kwa ajali na athari zake” alisema RPC Awadh
Wakizungumza kwa
nyakati mbalimbali katika kikao hicho bodaboda hao waliiomba Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwa nia ya kuandaa utaratibu ili waweze kuruhusiwa
kufanya kazi zao Visiwani hapo huku wakiahidi kuendelea kufuata sheria za
usalama barabarani.





0 Maoni