Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imekusanya sh. bilioni 48.4 tangu ilipoanza kukusanya tozo za miamala ya simu mwezi mmoja uliopita.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar-es-salaam amesema fedha zilizopatikana baada ya ukusanyaji wa tozo tangu sheria ilipoanza kutumika mwezi mmoja uliopita,  zimetumika kuboresha sekta ya afya,  elimu na miundombinu.

Hata hivyo amewasihi wananchi kuendelea kuvumilia suala la tozo za miamala wakati Serikali ikipanga kukutana na watoa huduma wa mitandao ya simu juu ya majadiliano ya kupunguza gharama za tozo kwa pande zote mbili.

Amesema tozo za miamala ya simu si michango ya kirafiki ni sheria iliyopitishwa na  Bunge baada ya kujadiliwa kwa kina  akibainisha kuwa wabunge ni wawakilishi wa wananchi.

Dkt. Nchemba ameongeza kuwa  nchi ndio zinavyojengwa hivyo amewapongeza watanzania wote ambao wanatoa mawazo mazuri ya kuboresha jambo hilo.