Mtu mmoja ameuawa kwa kupigwa risasi wakati wakaazi wa Kianjokoma huko Embu, kati mwa Kenya walipofanya maandamano juu ya kifo cha ndugu wawili mikononi mwa polisi.

Kwa siku mbili, wakaazi wa eneo hilo walifunga barabara na kutaka haki kwa familia ya Benson Njiru (22) na mdogo wake, Emmanuel Mutura (19).

Wawili hao walikamatwa katika mji wa Kianjokoma Jumapili usiku kwa madai ya kuwa nje kipindi cha marufuku ya kutoka nje cha saa nne usiku.

Familia yao imesema baada ya kuwatafuta katika vituo vya polisi vya karibu na eneo lao, bila matokeo, walipata miili yao katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali kuu ya Embu.

Polisi wanadai wawili hao waliruka kutoka kwa gari la polisi lililokuwa mbioni.

Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi (IPOA) imesema inachunguza vifo hivyo na imetuma maafisa wake katika eneo hilo. Mamlaka hiyo imeelezea wasi wasi kwamba vifo hivyo sio vya kwanza vinavyotokana na utekelezaji wa masharti ya Covid.

Makundi ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakilalamikia mauaji kadhaa ya kiholela nchini Kenya, mengine ambayo hayajatatuliwa kwa miaka. Ni maafisa wachache tu wa polisi ambao wamewahi kushtakiwa.