RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwepo kwa Tamasha la Kimataifa la
Filamu la Zanzibar (ZIFF), ni njia moja wapo ya kuukuza na kuutangaza utalii
pamoja na urithi wa Zanzibar.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu
Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Tamasha
la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF), ukiongozwa na Mkurugenzi wake
Profesa Martin Muhando.
Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alisema
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina unga mkono juhudi hizo zinazochukuliwa
na ZIFF ambazo alisisitiza kwamba ndio njia muhimu ya kuukuza na kuutangaza
utalii wa Zanzibar.
Akieleza kuhusu suala zima la uigizaji wa
Filamu kwa vijana, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ni vyema vijana wakapewa elimu
sambamba na kuunganishwa pamoja ili waweze kukuza na kuendeleza vipaji vyao
walivyonavyo katika tasnia mbali mbali.
Rasi Dk. Mwinyi alisema kuwa ni vyema ikawepo
sehemu maalum ya kutoa vipaji hasa ikizingatiwa kwamba vipaji hapa Zanzibar
vipo na kinachohitajika hivi sasa ni kuendelezwa tu na kutoa shukurani kwa ZIFF
kwa kuendeleza Tamasha hilo.
Rais Dk. Mwinyi pia, ameeleza haja ya
kuanzishwa kwa vyuo vya kuzalisha vipaji hapa nchini huku akisisitiza kwamba
kuwepo kwa semina zinazoendeshwa na ZIFF kutawasaidia kwa kiasi kikubwa vijana.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza
kwamba matamasha ya Kimataifa likiwemo Tamasha la Kimataifa la Filamu la
Zanzibar (ZIFF), ambalo kwa jina jengine linaitwa Tamasha la Kimataifa la Nchi
za Majahazi yanauwezo mkubwa wa kuutangaza utalii pamoja na kutangaza soko la
kuuza filamu.
Mapema Mkurugenzi wa Tamasha la Kimataifa la
Filamu la Zanzibar (ZIFF), Profesa Martin Mhando alimueleza Rais Dk. Mwinyi
kwamba Tamasha hilo lililoanza miaka 24 iliyopita na kuweza kuleta mafanikio
makubwa hapa Zanzibar ambalo linatarajiwa kufanyika kuanzia Julai 21 hadi 25
mwaka huu hapa Zanzibar.
Mhando amesema kuwa katika Tamasha la mwaka
huu filamu ya kwanza iliyoshinda ni kutoka Tanzania, lakini hata hivyo Tanzania
ilipoanza ilikuwa ikifanya filamu ndogo lakini kila siku zikiendenda mafanikio
zaidi yameonekana na kusema kwamba imefika wakati filamu zinazozalishwa nchini
ziwe na taaluma.
Aidha, alisema kuwa kati ya filamu 65 za mwaka
huu Tanzania ina filamu 16 na kumuhakikishia kwamba wanamatumaini makubwa ya
kupata zawadi kutokana na filamu hizo za Tanzania kuwa nzuri.
Alisema kuwa Tamasha hilo ni la muda mrefu na
limeweza kudumu kwa kiasi kikubwa hasa ikizingatiwa kwamba Tamasha la ZIFF ni
la pili kwa ukubwa katika bara la Afrika likitanguliwa na Tamasha la nchini
Bukina Fasso.
Pia, alieleza azma yao ya kuanzisha soko la
filamu hapa hapa Zanzibar kwani Zanzibar ni sehemu nzuri ya kutengeneza filamu
na imekuwa ikijitangaza na kujiuza wenyewe.
Alisema kuwa lengo kubwa walilokuwa nalo hivi
sasa ni kuiunganisha tasnia ya filamu na tasni ya utalii kufanya kazi moja ya
kuitangaza Zanzibar. Aliongeza kuwa mwaka huu katika mafunzo wanayoyafanya
yakiwemo mafunzo ya upigaji wa picha ambayo imejikita zaidi kwa vijana wa
Zanzibar ambao malengo makubwa ni kuutangaza uchumi wa Buluu sambamba na vijana
wenyewe kupata kipato.
Alisema kuwa mwaka huu kwa kushirikiana na
chuo cha DW cha Ujerumani wanafanya mafunzo ya filamu hasa kwa kuzingatia haja
ya kuwa na filamu zenye muendelezo, na ksuema kwamba wamepanga kuchagua hadithi
tano na kila hadithi italipwa dola za Kimarekani elfu kumi.
Aliongeza kwamba mwaka huu Tamasha
limejitahidi kuangalia upande wa wanawake kwani filamu inayofungua Tamasha
mwaka huu imetengenezwa hapa hapa Tanzania na aliyetengeneza ni mwanamke na
ndiyo filamu iliyochaguliwa kufungua Tamasha la ‘Pan African Film Festival
(PAFF)’ huko nchini Marekani.
Nae Bi Farida Nyamachumbe mratibu wa ZIFF
alitoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kuliunga
mkono Tamasha hilo tokea kuanzishwa kwake.




0 Maoni