Kigoma.
Vitendo vya ukatili wa
kijinsia kwa watoto vimebainika kukita mizizi katika wilaya ya Kibondo Mkoani
Kigoma ambapo ripoti ya Wilaya hiyo inaonesha kuwa Watoto 981 wamepewa ujauzito
Kigoma katika kipindi cha miezi sita iliyopita Januari mpaka Juni 2021.
Taarifa hiyo
imebainika wakati Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akiwa wilayani humo kukagua na kujionea utoaji
wa huduma za ustawi wa Jamii na masuala ya maendeleo ya jamii.
Naibu Waziri Mwanaidi
amesema taarifa hizo haziwezi kufumbiwa macho na badala yake watendaji
wanaohusika wafanye kila linalowezekana kuhakikisha watuhumiwa wanapatikana na
haki inatendeka katika kipindi kifupi iwezekanavyo.
Aidha Naibu Waziri
Mwanaidi ameongeza kuwa jamii haiwezi kutegemea miujiza ya mafanikio ya kizazi
kijacho endapo itabaki kufumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani
dhidi ya wanawake na watoto kwa kuangalia watoto wao wanapata mimba katika umri
mdogo na kukatisha ndoto zao.
Wakati huo huo
Naibu Waziri Mwanaidi amezindua Kituo cha huduma jumuishi kwa wahanga na
waathirika wa vitendo vya ukatili wa Kijinsia (One Stop Centre) katika
Hospitali ya Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma kitakachowawezesha walengwa wake
kupata huduma kwa pamoja na kwa muda mfupi na kuwataka maafisa Ustawi na
Maendeleo ya Jamii kushirikiana na vyombo vya dola kutoa elimu kwa kina dhidi
ya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.
Amesema kuwa kupitia
Kituo hicho ambacho kimefadhiliwa na Shirika la kimataifa la Save the Children,
kinajumuisha ofisi za polisi, maafisa ustawi, Daktari kitawezesha upatikanaji
wa huduma hizo kwa pamoja kwa waathirika ndani ya muda mfupi.
Kuhusu vitendo vya
ukatili dhidi ya watoto Naibu Waziri amesema kuwa Sheria ya Mtoto inataja
mashauri yao kukamilika ndani ya kipindi cha miezi sita lakini kwa mazingira ya
huduma za mkono kwa mkono kuna umuhimu wa kumaliza shauri ndani ya muda mfupi
zaidi.
Naye Afisa Ustawi wa
Jamii wa Halmashauri ya Wilaya Kibondo Sophia Gwamagobe amepongeza juhudi za
pamoja kati ya Serikali na wadau wa maendeleo katika kutafuta mwarobaini wa
matatizo miongoni mwa Watanzania ikiwemo kupambana na vitendo vya ukatili wa
kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto.
Kwa upande wake,
Mwakilishi wa Save the Children Jackson Nsabo amesema Shirika hilo limewiwa
kujenga kituo cha mkono kwa mkono ili kukabiliana na wimbi la vitendo vya
ukatili kwa wanawake na watoto.
Awali, Naibu Waziri
Mwanaidi alitembelea kikundi cha malezi chanya Wilayani Kibondo ambacho mbali
na kutoa ushauri nasaha kwa waathirika wa vitendo vya ukatili,
kinajishughulisha na ujasiriamali kwa kutengneza sabuni.
Akiwa kituoni hapo,
amewataka wazazi na walezi nchini kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto
wao ili kujenga taifa lenye ustawi kwa kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
Naibu Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis
amehitimisha ziara ya kikazi ya siku tano Mkoani Kigoma kwa kutembelea shughuli
za Maendeleo na Ustawi wa Jamii katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, Wilaya Kigoma
vijijini, Buhigwe, Kasulu na Kibondo.





0 Maoni