Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka Watendaji wanaofanya kazi ya ukusanyaji wa
maduhuli ya Serikali katika Minada, Mialo na Vituo vya Ukaguzi kufanya kazi
hiyo kwa uaminifu na uadilifu huku akionya kuwa hawataweza kuendelea kuwa na
Mtendaji atakayejihusisha na vitendo vinavyosababisha upotevu wa mapato ya
Serikali.
Waziri Ndaki aliyasema
hayo katika kikao cha Tathmini ya Ukusanyaji wa Maduhuli ya Serikali kwa mwaka
uliopita na kuweka malengo mapya ya ukusanyaji mapato kwa mwaka 2021/ 2022 kilichofanyika
jijini Dodoma Julai 23, 2021.
Akiongea na Watendaji
hao aliwaeleza bayana kuwa ili waweze kufikia malengo ya kukusanya Shilingi
Bilioni 90 walizojiwekea kukusanya kwa mwaka huu wa fedha ni lazima wafanye
kazi hiyo kwa uaminifu na uadilifu kinyume na hapo hawatafanikiwa kufikia
malengo.
"Katika kipindi
ambacho nimekuwa hapa Wizarani nimepata taarifa nyingi kuhusu baadhi yenu
kujihusisha na vitendo vya upotevu wa mapato, acheni kufanya hivyo kwa sababu
tukikugundua hatutaweza kuendelea na wewe," alisema Ndaki
Waziri Ndaki aliendelea
kusema kuwa Mhe. Rais, Samia Suluhu Hassan amewaahidi Watanzania mambo mengi
mazuri na ili mambo hayo yaweze
kutekelezeka yanahitaji Pesa, na miongoni mwa Pesa zinazotegemewa na Serikali
ni pamoja na zile zinazokusanywa kutoka kwenye minada, mialo na vituo vya
ukaguzi.
Aliendelea kubainisha
kuwa kwa mwaka huu atafuatilia kwa karibu utendaji kazi wa watendaji hao na
amepanga kukutana nao kila robo mwaka ili kupima utendaji kazi wa kila mmoja
ili kuona kama yale malengo yaliyowekwa yanafikiwa.
Aidha, Waziri Ndaki
aliwaelekeza Watendaji hao kupelekea taarifa ya minada isiyo rasmi ili aitambue
na kuifuta kwa sababu imekuwa ni kikwazo
kwa minada inayotambulika kisheria.
Pia aliwasisitiza Watendaji hao kuendelea
kufanya kazi ya Serikali kwa haki ikiwa ni pamoja na kuzuia uvuvi haramu na
utoroshaji wa mifugo kwani vitendo hivyo vimekuwa ni sehemu ya upotevu wa
mapato ya Serikali.






0 Maoni