Na Mwandishi wetu
Katika kukabiliana na
wimbi la mahabusu katika magereza mbalimbali nchini na kuwapunguzia mzigo Jeshi
la Magereza Serikali imeanzisha Operesheni Maalumu ijulikanayo kwa jina la
“Operesheni Punguza Mahabusu” ambayo inafanyika nchi nzima.
Hayo yamesemwa
leo na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo wakati
akizungumza katika kikao kilichohusisha Wafungwa na Mahabusu wanawake
katika Gereza Ruanda jijini Mbeya ambapo pia alitoa msaada wa vitu
mbalimbali ikiwemo magodoro, Taulo za Kike, Miswaki na sabuni kwa wafungwa na
mahabusu hao.
“Miongoni mwa mambo
ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassani
hapendi kuyaona ni mrundikano na muongezeko wa watu katika majela hasa wanawake
kwa kuwa anaamini wanawake ndio wanaojenga nchi na jamii wakishirikiana
na wanaume, kikubwa tunaichukua changamoto na tayari tunaanzisha operesheni
maalumu itakayoitwa Operesheni Punguza Mahabusu”
Aliongeza pia tayari
serikali imeanza kuyaendea mbio baadhi ya mambo ikiwemo changamoto ya kuchelewa
kwa upelelezi, utolewaji dhamana kwa kesi ndogondogo ambazo ndio zinaongoza kwa
kujaza mahabusu wengi katika magereza hali inayopelekea magereza kuhemewa na
mzigo mkubwa wa kulisha mahabusu.
Akizungumzia hali ya
msongamano katika Gereza hilo Mkuu wa Gereza la Wanawake, Mrakibu Mwandamizi wa
Magereza, Rehema Mwailunga alikiri kuwepo kwa msongamano ambao unasababishwa na
mkoa wa Mbeya kuwa na Mahakama ya kanda.
“Mheshimiwa Naibu
Waziri,nashauri ili kupunguza msongamano nashauri tuone umuhimu wa kujenga
bweni la wafungwa na mahabusu wa kike sambamba na hili lililopo hapa lakini
nakiri msongamano huu unasababishwa na kuwepo kwa mahakama ya Kanda hapa Mbeya
hivyo mahabusu na wafungwa wengi kutoka magereza ya wilaya wanakuja kusikiliza
kesi na rufaa zao hapa” alisema SSP Rehema
Naibu Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo akimkabidhi miche ya sabuni,Mkuu wa Gereza
la Wanawake Ruanda,Mrakibu Mwandamizi wa Magereza,Rehema Mwailunga kwa ajili ya
wafungwa.Naibu Waziri yupo jijini Mbeya kwa ziara ya kikazi ambapo
alipata fursa ya kuzungumza na kuwasikiliza wafungwa na mahabusu lengo ikiwa
kushughulika na msongamano wa mahabusu katika magereza mbalimbali nchini





0 Maoni