Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,
akizindua Chanjo ya Uviko 19 katika Viwanja vya Ikulu Jijini Dar es salaam leo
Julai 28,2021.Zanzibar
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo
tarehe 28 Julai, 2021 amezindua utolewaji wa chanjo ya UVIKO 19 na kuongoza
Watanzania kupata chanjo hiyo katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kabla ya kuanza zoezi hilo, Mhe. Rais Samia amewatoa hofu
Watanzania kuwa chanjo hiyo ni salama na yeye kama Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa
Majeshi ya Ulinzi na Usalama asingejitoa mwenyewe kujipeleka kwenye hatari huku
akijua kuwa ana majukumu makubwa yanayomtegemea.
“
Nimekubali kwa hiyari yangu kuchanja nikijua ndani ya mwili wangu nina chanjo
kadhaa ambazo nimeishi nazo kwa miaka 61 sasa, tangu tumezaliwa tumepata chanjo
zisizopungua tano na hii ya sita na nyingine nilizochanja nikiwa nasafiri, hivyo
sioni hatari ya chanjo hii baada ya wanasayansi kujiridhisha na zimekuja nchini
na wanasayansi wetu nchini wamejiridhisha mimi niko tayari kuchanja” amesema Mhe. Rais Samia.
Mhe. Rais Samia amewaomba Watanzania kwa hiyari yao kushiriki katika
zoezi hilo la chanjo hiyo ya UVIKO 19 ila waendelee kujihadhari na
ugonjwa huo.
Aidha, Mhe. Rais Samia amesema kama hujaguswa na maradhi hayo ya UVIKO 19
au watu wako wa karibu unaweza kubeza chanjo ila walioguswa wanatamani kupata
chanjo hiyo kwa haraka iwezekanavyo.
Amesema amekuwa akipokea jumbe mbalimbali za simu kutoka kwa baadhi ya
Watanzania wakimuuliza jinsi ya kupata chanjo hizo ambapo amesema kwa sasa
Serikali inaendelea kuratibu upatikanaji wa chanjo za kutosha ili kuwezesha
wananchi wengi kupata chanjo hizo.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na
Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewataka wananchi kuwapuuza wale wote
wanaopotosha kuhusu chanjo hizo za UVIKO 19 na kusisitiza kuwa ni salama kwa
afya baada ya wataalam wetu nchini kujiridhisha kabla ya kuamua kufanyika kwa
zoezi hilo.
Mhe. Dkt. Gwajima amewaomba viongozi wa dini, siasa na viongozi wengine
katika makundi mbalimbali na Watanzania kwa ujumla kupokea chanjo hiyo kwa kuwa
ni silaha ya kisasa katika kukabiliana na UVIKO 19.
Mhe. Waziri Dkt. Gwajima amebainisha kuwa nchi ambazo zimefanya zoezi
kama hili la uchanjaji zimepata matokeo
mazuri ikiwemo kupunguza maambukizi, kupunguza idadi ya wagonjwa wanaohitaji
kulazwa pamoja na kupunguza vifo
vitokanavyo na UVIKO 19.
Wakati
huohuo, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan amepokea
miradi iliyofadhiliwa na kujengwa na Serikali ya Ujerumani kupitia Jeshi la
nchi hiyo (GAFTAG) kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika hafla
iliyofanyika katika Hospitali ya Jeshi Lugalo Jijini Dar es Salaam.
Katika hafla hiyo, Mhe. Rais Samia na Amiri Jeshi Mkuu amesema miongoni
mwa miradi iliyokabidhiwa leo ni Idara ya Magonjwa ya Kuambukiza (Infectious Disease Department) ambapo
amesema msaada huo umekuja katika kipindi sahihi na muda muafaka kutokana na Dunia ikiwa ni
pamoja na Tanzania kukabiliwa na mlipuko wa magonjwa mengi ya kuambukiza,
ikiwemo UKIMWI, Kifua Kikuu, Malaria, Ebola
pamoja na UVIKO 19.
Mhe. Rais Samia amesema ujenzi wa Idara hiyo utaongeza uwezo wa nchi wa
kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza ambapo pia inaendana na dhamira ya
Serikali ya kuimarisha na kuboresha huduma za afya nchini pamoja na dhana ya
utalii wa kitabibu.
Aidha, Mhe. Rais Samia amesema miradi iliyokabidhiwa ni muendelezo wa
miradi mingi ambayo Serikali ya Ujerumani imefadhili nchini tangu mwaka 1961
kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Chuo cha Sayansi ya Tiba cha Jeshi (Military College of Medical Science),
Hospitali ya Jeshi Kanda ya Arusha, Idara ya Dharura ya Hospitali Kuu ya Jeshi
Lugalo, Ujenzi wa Mabweni ya wanafunzi katika Hospitali ya Kanda Bububu
Zanzibar pamoja na ujenzi wa Karakana ya kisasa ya kutengeneza Magari ya Jeshi.
Mhe. Rais ameihakikishia Serikali ya Ujerumani kuwa Tanzania itaendelea
kuenzi na kukuza zaidi uhusiano wa kirafiki na kihistoria kati ya mataifa haya
mawili na kulitaka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kutunza miradi hiyo ili
iendelee kutoa huduma kama ilivyokusudiwa.
Vilevile, Mhe. Rais Samia ameipongeza JWTZ kwa kazi nzuri ya kulinda
mipaka ya nchi na kuiwakilisha vyema nchi kimataifa kwenye misheni mbalimbali
za kulinda amani.
Hafla ya makabidhiano ya miradi mbalimbali iliyofadhiliwa na Serikali ya
Ujerumani kwa Jeshi la Tanzania imehudhuriwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi
Jenerali Venance Mabeyo, Mhe. Balozi wa Ujerumani nchini Bibi Regine Hess, Mkuu
wa Kikundi Maalum cha Ushauri wa Kijeshi kwa Tanzania (GEFTAG) Luteni Kanali Thomas Nalbach, Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii ,Jinsia , Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima
pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akipata Chanjo ya Uviko 19 katika Viwanja vya Ikulu Jijini Dar es salaam leo Julai 28,2021. Picha na Ikulu.






0 Maoni