Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar ZAFELA inatarajia kufanya kongamano la kitaifa kuhusu udhalilishaji wa kijinsia pamoja na uzinduzi wa mfumo wa ukusanyaji wa taarifa za kesi za udhalilishaji ulionzishwa na jumuiya hiyo.
Akizungumza na
Waandishi wa Habari katika ofisi za ZAFELA Mpendae, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo
Safia Hija Abras amesema Jumuiya imeandaa mfumo mpya wa ukusanyaji data
ili kuipima utendaji kazi katika utetezi wa maswala ya
Udhalilishaji ambao utasaidia kuondoa mgongano wakati wa kutoa taarifa za
kesi zilizoripotiwa baina ya taasisi moja na nyengine .
Bi safia alieleza kuwa
kila taasisi inayosimamia kupiga vita vitendo vya udhalilishaji itaweza kutumia
mfumo huo ili kuepuka kujirejea kwa taarifa wakati wa uwasilishaji wa kesi
hizo.
“Katika utendaji wa
kazi zetu tumeona ili tuweze kupima na kujipima jinsi gani utetezi unafanyika
katika masuala ya udhalilishaji ni vyema kuwa na mfumo maalum amabao utakuwa
unakusanya data hii itaepusha utofauti wa kuripoti kiwango cha taarifa za
udhalilishaji kutoka taasisi moja na nyengine” alisema Mwenyeiti.
Mwenyekiti huyo
alifahamisha kuwa kupitia kungamano hilo watapata nafasi ya kutoa taarifa
za utekelezaji, mafanikio na changamoto wanazokumbana nazo kuanzia kipindi cha
Januari hadi sasa katika kuhakikisha kwamba wanafikio lengo la jumuiya
hiyo la kutokomeza vitendo hivyo vya udhalilishaji wa kijinsia nchini.
Nae Mkurugenzi wa
Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar ZAFELA Jamila Mahmoud amesema jamii
imekuwa na muamko mkubwa wa kufika katika vituo vya sheria katika kutoa
malalamiko ambapo kutoka mwaka 2020 hadi 2021 jumuiya hiyo imepokea
kesi zaidi ya 100 za vitendo vya udhalilishaji.
Kongamano hilo
ambalo linalotarajiwa kufanyika Julai 28, katika Ukumbi wa Idrisa Abdulwakil
litajumuisha Asasi za kiraia na taasisi za Serikali ikiwemo jeshi la
Polisi, na watendaji wa Mahkama ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi.





0 Maoni