RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amelipongeza Tamasha la “Nandy Festival” na kusema kwamba kufanyika kwa Tamasha hilo hapa nchini ni fursa ya kuutangaza utalii wa Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokuwa akizungumza na wasanii wa Tamasha la “Nandy Festival” waliopo hapa Zanzibar wakiongozwa na mwanamuziki maarufu wa muziki wa kizazi kipya  Faustina Charles Mfinanga maarufu Nandy.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi aliupongeza utayari wa wasanii  wa tamasha la “Nany Festival” kwa kuja Zanzibar na kufanya maonyesho hatua ambayo alisema ni faraja kwani maonyesho hayo yataendelea kuitangaza zaidi Zanzibar.

Alieleza jinsi alivyofurahishwa na  na hatua hiyo na kueleza kwamba ataendelea kushirikiana na wasanii hao na kila itakapowezekana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa tayari kutoa msaada utakaohitajikwa kwa lengo la kuitangaza Zanzibar na kuinua vipaji vya wasanii wake hasa ingazingatiwa kwamba tayari wasanii wa Tanzania Bara wamepiga hatua kubwa katika tasnia hiyo ya muziki.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa licha ya kuwepo kwa matamasha mengi hapa Zanzibar lakini pia kufanyika kwa matamasha kama hayo ya “Nandy Festival” ni fursa ya kuyaendeleza matamasha kwani lengo ni kuwa na matamasha mengi ambapo ndani ya miezi yote 12 kukawepo matamasha na baada ya hapo kila mwezi ni vyema yawepo hata matamasha mawili.

Rais Dk. Mwinyi aliongeza kuwa matamasha yana umuhimu mkubwa sana kwa sababu yanaleta watu kutoka nje na kusema kwamba muziki wa kizazi kipya nao unaweza kuleta watu wengi hapa nchini.

Nae mwanamuziki nguli wa kizazi kipya hapa nchini Faustina Charles Mfinanga maarufu Nandy alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba yeye na wasanii aliokuja nao kwa ajili ya Tamasha lake la “Nandy Festival”,wamepata mapokezi makubwa hapa Zanzibar.

Alisema kuwa mbali ya kufanya tamasha hilo pia, wakiwa hapa Zanzibar walipata fursa ya kutembelea vivutio kadhaa vya utalii vilivyopo hapa nchini.

Aidha, Nandy aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya kwa kuwa nao karibu tokea alipowasili yeye na wasanii wenzake hapa Zanzibar kwa ajili ya tamasha la “Nandy Festival”.

Alisema kuwa Tamasha la “Nandy Festival” lilianza mwaka 2019 na kuweza kuzunguka Tanzania nzima wakati huo na mwaka uliofuata hawakuweza kufanya hivyo kutokana na kuwepo kwa maradhi ya COVID 19, lakini mwaka huu wameweza kuendelea na tamasha lao hilo na walishatembelea mikoa ikiwemo Kigoma, Mwanza, Dodoma na Arusha na hivi sasa kupata nafasi ya kuja Zanzibar.

Aliongeza kuwa tamasha hilo limekuwa likisaidia kwa kiasi kikubwa hasa kwa vijana kuweza kupata ajira kutoka makundi kadhaa akisema kwamba lengo ni kukuza muziki wa kizazi kipya barani Afrika.

Nandy aliahidi kushirikiana na wasanii wa Zanzibar ili kuupeleka mbele muziki wa kizazi kipya huku akieleza kwamba ipo haja ya kushikwa mkono na Serikali katika kuhakikisha wanafanikisha zaidi matamasha yao.