Mjumbe wa kamati kuu ya Halmashauri kuu ya
chama cha Mapinduzi Taifa Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amesema chama cha
Mapinduzi kina matumaini makubwa na Jumuiya za chama katika kufanikisha
Fikra,mikakati na mitazamo ya kuwaandaa vijana wake kushika nafasi za uongozi.
Mjumbe huyo wa kamati kuu ya Halmashauri kuu
ya CCM Taifa alieleza hayo wakati akifungua mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa
vijana wa chama cha Mapinduzi(UVCCM) Mkoa wa Mjini uliofanyika katika ukumbi wa
Zanzibar Ocean View Hotel uliopo kilimani.
Alisema wajibu wa wanachama wa chama cha
Mapinduzi pamoja na Jumuiya zake zina jukumu la kuhakikisha CCM inashinda
katika chaguzi zote kama ilivyo elezwa ndani ya katiba ya chama ibara ya 5(1)
ikiwemo kushinda uchaguzi wa Serekali kuu na Serekali za mitaa kwa upande wa
Tanzania Bara.
“Mnapaswa kuelewa kuwa Jumuiya za chama cha
Mapinduzi zimeundwa ili kuisaidia CCM, UVCCM Ikiwa ni moja ya Jumiya hizo ina
Jukumu la kutimiza malengo ya CCM “Alisema Mhe.Hemed.
Aliwakumbusha wasimamizi wa Jumuiya hiyo ya
Umoja wa vijana kutosahau wajibu wao wa kuwaandaa vijana ili wawe viongozi Bora
wa baadae kupitia chama na Serekali sambamba na kulinda,kutetea,pamoja na
kushawishi vijana wengine kujiunga na chama hicho.
Alieleza kuwa, suala la Serekali inayo
tekeleza Ilani ya CCM kuwapa nafasi za uongozi vijana ni jambo lisilo epukika
kwa kuzingatia mahitaji ya jamii na uwendeshaji wa Nchi kuhitaji vijana wenye
uweledi waliopikwa kupitia chama cha Mapinduzi.
Mhe.Hemed aliwaeleza vijana wa UVCCM kwamba,
chama cha Mapinduzi kupitia Serkali zake zote mbili kimetoa nafasi nyingi za
uongozi kwa vijana ambapo Mara Rais wote wawili kupitia teuzi zao wameonesha
jinsi walivyojenga matumaini na kuwapa nafasi za uongozi vijana wanaotokana na
chama cha Mapinduzi.
“Napenda niwathibitishie vijana wote
walioteuliwa wameonesha ujuzi,maarifa na uwezo wa uongozi katika nafasi
walizopewa,Hivyo naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza sana UVCCM kwa weledi
na kuiva kiuongozi”Alieleza Mjumbe huyo wa kamati kuu.
Makamu wa Pili wa Rais Mhe.Hemed alisema bado
ipo haja ya kuwapa fursa vijana kupitia chaguzi mbalimbali hususani majimboni
ili chama kiendelee kuwaanda vijana waweze kushika nafasi za uongozi.
“Sisi katika chama chetu hatuoni vijana ni tishio
la uongozi bali ni chachu ya kuharakisha utendaji kazi kupitia Nyanja zote za
kisiasa na kiuchumi”Alisema Makamu wa Pili wa Rais.
Akisoma risala kwa niaba ya vijana hao wa
UVCCM Mkoa wa Mjini Katibu wa Vijana wilaya ya Mjini Ndugu Ramadhani Abass Mcheju
alimueleza mgeni rasmi kuwa Umoja wa vijana wa chama cha Mapinduzi ni chombo
cha kuwaunganisha vijana pamoja kwa lengo la kuwapatia taaluma itakayowasaidia
katika harakati za maisha yao ya kila siku.
Alisema Mkutano huo wa Baraza kuu la Umoja wa
Vijana Mkoa wa Mjini pia utajadili na kutathimini siku mia moja (100) za Mama
Samia tangu angie madarakani ambapo wamefarajika sana na imani alioionesha kwa
kuwateua vijana kuwakabidhi dhamana ya Uongozi.
Katika risala yao vijana hao walimpongeza Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa
mkakati aliokuja nao wa kudhibiti mapato ya serikali na kuhakikisha anaziba
mianya yote ambayo watumishi wasiokuwa waaminifu hutumia kwa kujinufaisha
binafsi.
Kuhusiana na Changamoto zinazoikabili Jumuiya
ya Umoja wa Vijana Mkoa wa Mjini walisema umoja huo unakabiliwa na
changamoto ya kukosekana kwa maeneo kwa ajili ya kujenga nyumba za watendeji wa
Jumuiya.
“Ndugu mgeni rasmi aliekuwa Mwenyekiti wa
UVCCM Taifa ndugu Heri Denis James alitoa agizo kujengwa kwa nyumba za
watendaji lakini hapa kwetu bado tunasuasua katika utekelezaji wa agizo hilo
kwa kukosa maeneo ya kujenga nyumba hizo”. Alisema Katibu Mcheju
Nae, Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM anaefanyia
kazi zake Zanzibar ndugu Mussa Haji Mussa alimuhakikishia Mjumbe wa kamati kuu
ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba kufuatia uchaguzi mdogo
wa jimbo la konde Unatarajiwa kufanyika Julai 18 mwaka huu umoja wa vijana
utahakikisha ushindi wa jimbo hilo unapatikana mchana kweupe.
Vile vile, Ndugu Mussa aliwaomba vijana wa
umoja huo kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbali mbali kufuatia uchaguzi wa
chama kupitia ngazi tofauti unaotarajiwa kufanyika mapema mwaka ujao pamoja
kuepuka tabia ya kutengeneza makundi yatakayosababisha kudhofisha maendeleo ya
Jumuiya hiyo na chama kwa Ujumla.
Mapema, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameongoza kikao cha kwanza cha Tume ya uratibu na
udhibiti wa dawa za kulevya Zanzibar tangu alipoteuliwa kushika nafasi hiyo.




0 Maoni