WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuboresha miundombinu ya bandari ili kuvutia idadi kubwa ya watumiaji zikiwemo nchi za ukanda wa Maziwa Makuu.
Ameyasema hayo leo
(Jumanne, Julai 20, 2021) alipokutana na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi
Leonard Chamuriho, Mkurugenzi wa Bandari, TASAC, TBS, TMDA, Kamishna wa Forodha
pamoja na wadau mbalimbali wa masuala ya usafirishaji.
Amesema lengo la kikao
hicho ni kufanya tathmini ya hatua zilizofikiwa katika uboreshwaji wa huduma
mbalimbali bandarini zikiwemo za upakuaji wa mizigo.
Waziri Mkuu amesema
Serikali imejipanga kununua vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha kuwa
mizigo yote inayopitia bandarini inapakuliwa katika kipindi cha muda mfupi.
Amesema bandari za Dar
es Salaam, Mtwara na Tanga zimefanyiwa maboresho makubwa, hivyo amewasisitiza
wadau wa sekta binafsi waendelee kuleta meli za kutosha.
Waziri Mkuu amesema
mbali na maboresho yaliyofanyika katika bandari hizo, pia bandari za Kabwe,
Kasanga nazo zimeboreshwa pamoja na ujenzi wa bandari ya Karema ili kurahisisha
usafirishaji wa mizigo na abiria katika nchi za Congo, Zambia na Burundi.
Naye,
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Chamuriho amesema kuwa ujenzi ndani ya
bandari ya Dar es Salaama unaelekeka kukamilika “Gati zote saba tumezimaliza na
sasa tunamalizia eneo la makontena katika gati namba sita na saba ambalo
litakamilika mwezi Agosti, 2021, hii itasaidia kuongeza ufanisi ndani ya
bandari”
Pia ameongeza kuwa
wataendelea kuzingatia masuala yote ya kisheria, kisera, kiutawala na
kiutendaji na kuyasimamia kikamilifu kwa lengo la kuongeza ufanisi katika
uendeshaji wa bandari ili kila anayeitumia aweze kunufaika.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli
Tanzania, Msanja Kadogosa amesema kuwa Shirika hilo limefanikiwa kukarabati
mabehewa zaidi ya 200 ya mizigo ambayo yanaenda nchi za Burundi na Kongo.
Kadogosa ameongeza kuwa
katika mwaka huu wa fedha, Serikali imelitengea Shirika hilo bajeti kwa ajili
ya kukarabiti mabehewa 660 na kazi ya ukarabati itaanza muda wowote, pia vichwa
vingine tisa vitakarabtiwa kwa ajili ya kutoa huduma ya usafirishaji wa mizigo.
Akizungumzia kuhusu
usafirishaji wa mafuta nchini Uganda, Kadogosa amesema kuwa wameanza kutekeleza
zoezi hilo ambalo lilikwama kwa takribani miaka 15 na wiki ijayo watapeleka
lita milioni moja kwenda nchini Uganda.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti, wadau wa sekta ya bandari wameipongeza Serikali kwa hatua
mbalimbali inazochukua katika kuboresha sekta hiyo na wameshauri hatua zaidi
zichukuliwe ili kuvutia zaidi watumiaji wa bandari nchini.





0 Maoni