Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Hamisi Issa

Njombe.

 Mwanaume mmoja ajulikanae kwa jina la Benitho Mbatha(23) Konda wa Daladala amefariki Dunia Chuambani akiwa na Mpenzi wake Jazila Said (27) Mkazi wa Namtumbo, chanzo kikielezwa kuwa ni jiko la Mkaa

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Hamisi Issa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema Konda huyo wa Daladala na Mpenzi wake waliingia na Jiko la Mkaa ndani ya chumba cha kulala kwa lengo la kupunguza Baridi kali inayoendelea Mkoani Njombe.

Kamanda Hamisi amesema tukio hilo limetokea Tarehe 17 mwezi huu majira ya saa Tano za Usiku Mtaa wa National Housing Kata ya Njombe Mjini wakiwa wamelala katika chumba kimoja hata hivyo hakuna mtu aliegundua mapema taarifa za Kifo hicho.

Amesema Sababu ya kifo chao inaonyesha wakati wakiwa hai waliweka moto wa mkaa kwa ajili ya kujihifadhi na baridi na huu mtindo wa kuweka mkaa kwa watu wa Njombe ni mtindo ambao umeshazoeleka.

Katika hatua nyengine Kamanda Hamis amewataka wananchi wa Mkoa wa Njombe kutumia njia nyingine kujikinga na baridi na si kuingia na Jiko ndani kama ambavyo wengi wamekuwa wakifanya kwani kufanya hivyo ni hatari kwa maisha yao.

Kamanda Hamis ameeleza tukio hilo ni la Tatu kutokea Njombe kutokana na tukio jingine kumkuta Dada Mkazi wa Songea aliyekuwa mhudumu wa baa moja mjini Njombe kufariki ndani kwa jiko la mkaa huku mwingine akifariki Wilayani Wanging’ombe kwa jiko la mkaa.

Amani Samsoni ni mmiliki wa Nyumba aliyokuwa akiishi marehemu Benitho Mbata huku akiwa ni mtu wa kwanza kushuhudia tukio hilo baada ya yeye kwenda kumtembelea marehemu na kuwaona wote wawili wakiwa wamefariki

“Lakini bado mimi nilifuatilia kwa majirani wanasema yule mwanamke alikuwa anaelekea Madaba,alikosa nauli na huyu kijana kwa kuwa yupo pale kwenye magari akamwambia njoo upumzike kwanza na kesho nitakusaidia nauli ya kukufikisha kwenu kwa hiyo hiki kitu kinahuzunisha sana”alisema Amani Samson