Waziri
Mkuu Kaasim Majaliwa ameipa siku saba za awali tume aliyoiunda kuchunguza
chanzo cha moto katika soko la kimataifa la Kariakoo ili kubaini nini
kimesababisha au nani kasababisha moto huo.
Ametoa
kauli leo (Jumapili Julai 11, 2021) alipokuwa anaongea na wafanyabiashara na
wakazi wa eneo la Kariakoo baada ya kukagua hatua zinazoendela kuchukuliwa
kudhibiti moto huo, Jijini Dar es Salaam.
Amesema
kuwa kamati iliyoundwa ambayo itafanya kazi na kamati ya ulinzi na usalama
iliyoanza kufanya kazi chini ya Mkuu wa Mkoa huo itajumuisha Ofisi ya
Rais-Ikulu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo itawakilishwa
na Mkurugenzi wa Maafa.
Wengine
ni Vyombo vya Ulinzi na Usalama ikujumuisha Jeshi la Wananchi, Jeshi la Polisi,
Zimamoto pamoja na Taasisi ya Kupambana na Rushwa. Pia Waziri Mkuu alizitaja
Wakala wa Majengo, Shirika la Umeme (TANESCO), Mwanasheria Mkuu wa Serikali
pamoja na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)
“
Endapo itagundulika kama kuna mtu alihusika kwa namna moja au nyingine, hatua
kali za kisheria zitachukuliwa moja kwa moja, kitendo cha kuungua kwa soko hili
la miaka chungu mzima lazima kuwe na uchunguzi wa kina, kwanini leo lishike
moto”
Aidha,
Waziri Mkuu amewataka wafanyabiashara katika soko hilo wawe watulivu wakati
Serikali inafanya kazi yake ya kujua chanzo cha moto huo na amewahakikishia
usalama wa mali zilizo ndani ya soko hilo
Waziri
Mkuu pia aliwataka wafanyabiashara kutoingia ndani ya soko hilo katika kipindi
hiki ambacho udhibiti unaendelea hadi pale timu zilizoundwa zitakapojiridhisha
na utulivu na kufanya sensa ya watu wenye mali kuingia mmoja baada ya mwingine
ili wakatoe vitu walivyoviacha
“Tunachoshukuru
kule chini shimoni hakuna moto, mali zote zinalindwa, msiwe na mashaka milango
yote imefungwa na makamanda wako ndani na nje wanalinda, mali zote
zimehifadhiwa, msiwe na mashaka”
Kadhalika
Waziri Mkuu amewaahidi wafanyabiashara hao kuwa Serikali itaongea na Mabenki
yaliyowakopesha wafanyabiashara waliounguliwa na mali zao kuwaongezea muda wa
kulipa mikopo yao baada ya kuunguliwa.
“Tume
itapata taarifa za kila mmoja mwenye mkopo rasmi kwenye taasisi za fedha ili
tuzungumze nao waongeze muda waache kipindi hiki ili uweze kulipa hapo baadae
utakapo kuwa umetulia,biashara imeungua naamini mabenki yatatuelewa na kuweka
utaratibu mzuri”





0 Maoni