Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiweka jiwe la Msingi la ujenzi wa Mabweni ya wanafunziwa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kampasi ya Karume Zanzibar.

Zanzibar

Kiasi cha Shilingi Bilioni Kumi na Tano na Milioni Mia mbili (15.2)kina hitajika kwaajili ya ujenzi wa Mabweni ya Wanafunzi  wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere – Kampasi ya Karume Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameeleza hayo kupitia hotuba alioisoma kwa niaba ya Rais Dk. Hussein Mwinyi  katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la mradi wa ujenzi wa Mabweni ya wanafunzi  wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere – Kampasi ya Karume Zanzibar, Bububu Mkoa wa Mjini Magharib .

Amesema ni vema wadau wakaunga mkono juhudi za Serikali katika kuchangia Ujenzi wa Mabweni hayo ambao yakikamilika yatasaidia wanafunzi kupata malazi bora na salama na hatimaye kupata ari ya kusoma ili kupata maarifa bora yatakayoongeza maendeleo kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Katika hatua nyengine Mh Hemed amemwagiza mkandarasi anaetekeleza Mradi huo SUMA JKT kuhakikisha mradi huo unajengwa katika ubora unaokubalika na kukamilika kwa  wakati uliopangwa ili kutatua changamoto ya Makaazi inayowakabili wanafunzi.

Amesema uwepo wa Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu  Nyerere visiwani Zanzibar  ni kielelezo Chanya katika kuenzi na kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa Vitendo.

Awali Waziri wa Elimu na Mafunzo ya amali Zanzibar Mhe. Simai Mohamed Said amesema Wizara hiyo itahakikisha inaendelea kushirikiana na chuo hicho huku ikizingatiwa kuwa Wizara anayoingoza ipo katika mchakato wa kufanya marekebisho kupitia kitengo chake kinachosimamia elimu ya juu ili kiweze kwenda sambamba na Wadau wa Elimu Nchini.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila  amesema Kampasi ya Karume imefanikiwa kutenga fedha kupitia bajeti yake ikiwa na adhmna ya kutekeleza miradi mbali mbali ikiwemo ujenzi wa Mabweni ya wanafunzi, Ujenzi wa madarasa ya kusomea, Ujenzi wa Ofisi kwa upande wa Pemba pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu.

Akisoma Taarifa ya utekelezaji wa mradi huo  Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la uzalishaji Mali la jeshi la kujenga Taifa (SUMA-JKT) Kanali Absolonon Lyanga Shausi alisema wanaishukuru serikali ya mapinduzi Zanzibar kupitia wakala wa majengo Zanzibar kwa kuisajili SUMA-JKT kuweza kufanya kazi zake Zanzibar na kuahidi kuwa mradi huo utakamilika ndani ya wakati uliopangwa wa kipindi cha miezi 18 huku ikizingatia weledi katika utekelezaji wake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed akipata maelezo ya mradi wa ujenzi wa Mabweni ya Wanafunzi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Karume Zanzibar kutoka kwa Mkurugenzi wa Huduma za ushauri wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Msanifu Majengo Wencelause P. Kizaba
Mkuu wa chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila akimueleza Mgeni Rasmi changamoto zinazokikabili chuo hicho ikiwemo uvamizi wa eneo la chuo katika hafla ya uwekaji wa jiwe la Msingi la ujenzi wa Mabweni ya wanafunzi kampasi ya karume Zanzibar