Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema kuwa watumishi wa umma kama watazingatia
kanuni za utumishi wa umma basi utumishi wa umma utafanyika kwa kiwango cha juu
katika kuwapa huduma Watanzania katika sekta mbalimbali nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya
Utawala na Rasilimaliwatu wizarani hapo Bi Zahara Guga wakati akizungumza na
watumishi wa wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma.
Akizitaja kanuni hizo; kutoa huduma bora, utii
kwa Serikali, bidii ya kazi, kutoa huduma bora bila upendeleo, kufanya kazi kwa
uadilifu, kuwajibika kwa umma pamoja na kuheshimu sheria na matumizi sahihi ya
taarifa.
“Panapokuwepo na matumizi sahihi ya taarifa
ambayo ni miongoni mwa kanuni zetu za utumishi hapatokuwepo suala la kuvuja kwa
siri za Serikali, jambo ambalo kama litazingatiwa linaweza kuzuia matatizo
mengi ambayo yanaweza kumkumba mtumishi hadi kufukuzwa kazi” amefafanua Bi
Guga.
“Kwa nini mtumishi wa umma afike huku kubwa ni
kutii sheria na kanuni zake tu si kingine” ameongeza Mkurugenzi Msaidiizi huyo
wa Wizara ya Habari.
Kwa sasa taifa letu
lina idadi ya watu inayokadiriwa takriban milioni sitini huku watumishi wa umma
wakiwa ni laki tatu tu, na waumishi wa wizara hiyo ni wawakilishi wa Watanzania
wengine. Aidha, Bi Guga amesisitiza watumishi hao wakumbuke wanawawakilisha
watumishi wengine na wananchi ambao ndiyo wanaolipa kodi na fedha hiyo ndiyo
inayotumika kulipa mishahara kwa watumishi wa Serikali.
“Suala la kufanyiwa
kazi kwa siku mbili lifanyike kwa siku mbili na siyo mwezi mzima, hapo utakuwa
umetimiza wajibu wako na umefanya kazi kwa bidiii na ukiwa mtumishi wa umma
kuwajibika kwako ni wajibu na siyo hisani kwa wale wanaokuja kuhudumiwa”
amesema Bi Guga.
Wafanyakazi wa wizara hiyo mara baada ya kikao
hicho wamesema kuwa vikao vya namna hiyo vifanyike mara kwa mara hatua
itakayowapa watumishi nafasi ya kuuliza maswali na kujibiwa ili kusaidia
kuondoa malalamiko yasiyo ya lazima.
“Hili ni juma la
Utumishi wa Umma na tumejifunza mengi ninakumbuka awali niliwahi kuona
maadhimsho ya utumishi wa umma katika viwanja vya Mnazi Mmoja huko Dar es
Salaam, kwa ujumla mimi binafsi nitaongeza juhudi katika kazi ili niweze kuwa
mfanyakazi wa mfano bora huko mbeleni” alisema Julius Mgaya kutoka Idara ya
Sera na Mipango ya wizara hapo.
.




0 Maoni