Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akishiriki Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa
Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC unaofanyika
katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Joaquim Chissano uliopo Maputo nchini
Msumbiji leo tarehe 23 Juni, 2021.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 23 Juni, 2021 ameshiriki Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika mjini Maputo nchini Msumbiji.
Mkutano huo umejadili ajenda mbalimbali zikiwemo zinazohusu mtangamano wa
nchi wanachama wa jumuiya hiyo, fursa mbalimbali za kiuchumi, pamoja na
changamoto za kiusalama.
Mwenyekiti wa SADC ambaye pia ni Rais wa Msumbiji
Mhe. Filipe Jancinto Nyusi amesema jitihada za pamoja kutoka nchi wanachama wa
ukanda wa SADC zinahitajika zaidi katika kukabiliana na tatizo la ugaidi
linaloikabili nchi hiyo, kwani limekuwa likirudisha nyuma juhudi za maendeleo kwa
Msumbiji na nchi wanachama.
Aidha, masuala mengine yaliyojadiliwa katika mkutano
huo wa dharura ni maambukizi ya Ugonjwa
unaosababishwa na virusi vya Corona (UVIKO 19), uanzishwaji wa kituo cha
majanga, masuala ya mabadiliko ya tabianchi, usalama wa chakula, biashara na
Uwekezaji katika ukanda wa Jumuiya hiyo ya SADC.
Rais Nyusi amezisisitiza nchi wanachama kuendelea
kuunga mkono jitihada za Taasisi za Utafiti
katika kufuatilia taarifa za kusambaa kwa UVIKO 19 na mawimbi mapya ya
ugonjwa huo na kuendelea kuchukua tahadhari ili kuzuia maambukizi mapya.
Kuhusu changamoto za tabianchi, Mhe. Rais Nyusi
amesema baadhi ya nchi wanachama zimekumbwa na uhaba wa mvua na nyingine kupata
mvua nyingi zaidi na kufanya uwepo wa uwezekano kwa baadhi ya nchi kukumbwa na
uhaba wa chakula.
Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa
Jumuiya ya Maenendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), umefanyika sambambana na
maadhimisho ya miaka arobaini tangu kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo, ikiwa na kauli
mbiu “ Kuimarisha Amani na Usalama,
Kuhamasisha Maendeleo na Ustahamilivu wa Changamoto Zinazoikabili Dunia”.
Mhe. Rais Samia amemaliza ziara ya kikazi ya siku
mbili nchini Msumbiji na kurejea Jijini Dodoma nchini Tanzania.





0 Maoni